Viongozi wa nchi 7 tajiri duniani wameahidi kutenga kiasi cha dola bilioni 600 kwa ajili ya kujenga miundo mbinu ya kupamabana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi. Mradi huo unazingatiwa kuwa jibu la nchi za magharibi kwa uwepo wa China katika nchi zinazoendelea. Mwenyeji wa mkutano wa nchi hizo tajiri kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema nchi za G 7 zitafanya juhudi za kujenga ushirikiano wa karibu na nchi zinazoendelea ikiwa ikiwa pamoja na bara la Afrika. Kansela wa Ujerumani ameeleza kuwa nchi saba tajiri zinakusudia kujenga ushirikiano na nchi zinazoendelea siyo kwa ajili ya hisani tu bali kwa ajili ya manufaa ya pande zote. Kwa upande wake rais wa Marekani Joe Biden amesema vitega uchumi vitakavyowekwa vitaelekezwa katika kuimarisha uchumi wa nchi zote na kwa ajili hiyo Marekani imeahidi kutenga dola bilioni 200 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Wakati huo huo Marekani inapanga kupeleka silaha za ulinzi wa anga nchini Ukraine. Kwa mujibu wa taarifa Marekani itanunua silaha hizo kutoka Norway. Silaha hizo za ulinzi ndizo zinazotumika kwa ajili ya ulinzi wa eneo la ikulu ya Marekani. Marekani pia itaipelekea Ukraine silaha za aina nyingine. Viongozi wa G7 wanaohudhuria mkutano huo leo wataujadili uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Vile vile viongozi kutoka Afrika, Argentina, India na Indonesia watashiriki kwenye vikao vya leo ambapo suala la ulinziwa mazingira litawekewa mkazo.