Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma anapanga kupinga ripoti ya mahakama kuhusu uchunguzi wa ufisadi mwingi uliojitokeza katika utawala wake wa miaka tisa. Msemaji wa Zuma amewaambia waandishi wa habari kaskazini mwa Johannesburg kwamba Zuma mwenye umri wa miaka 80, anachukulia yaliyomo kwenye ripoti hiyo kukosa mantiki sana. Msemaji huyo amesema uchunguzi wa wizi wa takriban dola bilioni 30 kutoka katika kampuni za serikali, umejaa uwongo, porojo, na hauna uthibitisho kamili. Ripoti hiyo iliyochapishwa Jumatano, ilimtuhumu Zuma kuhusika pakubwa kwenye sakata hilo, linalodaiwa kunufaisha pakubwa familia bwenyenye ya Gupta miongoni mwa wengine.