Wanaharakati Morocco wataka uchunguzi kuhusu vifo vya wahamiaji

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wa Morocco AMDH, wametaka uchunguzi ufanywe kufuatia vifo vya wahamiaji 23 wa kiafrika walipokuwa wakijaribu kuingia katika uzio wa Melilla nchini Uhispania. Kundi hilo la AMDH limewashutumu walinzi wa mipaka wa Morocco kwa kutumia nguvu nyingi isiyohitajika dhidi ya wahamiaji. Vifo hivyo vilitokea Ijumaa baada ya wahamiaji 2,000 kuuvamia uzio wa mpakani unaotenganisha mji wenye mamlaka yake ya ndani wa Uhispania Melilla na Morocco. Kulingana na maafisa wa Morocco, takriban wahamiaji 500 walifaulu kuingia eneo linalodhibitiwa la mpakani, na wengine wasiopungua 18 walifariki. Akizungumza mjini Brussels, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alielekeza lawama kwa makundi ya uhalifu yanayosafirisha wanadamu kinyume cha sheria. Jaribio hilo la kuvuka mpaka lilikuwa la kwanza tangu Uhispania na Morocco ziliporejesha uhusiano wao wa kidiplomasia mwezi uliopita.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii