Marais wa EAC waunda kikosi cha kulinda amani DRC

MARAIS wa Afrika Mashariki wameidhinisha kuundwa kwa kikosi maalum cha kudumisha amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Katika mkutano uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi, marais hao waliagiza kwamba wanajeshi wa kikosi hicho maalum cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) watumwe kudumisha amani katika taifa hilo linalokumbwa na misukosuko. Wanajeshi hao wanatarajiwa kushirikiana na wanajeshi wa DRC pamoja na walinda usalama wengine, katika kufanikisha majukumu yao.

“Marais wamekubali na kuhusu mahitaji yote yatakayowezesha shughuli za kikosi cha Usalama cha Kikanda na matawi yake yote,” ikasema taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo wa marais walikutano chini ya uenyekiti wa Rais Uhuru Kenyatta.

Taarifa hiyo ilisema kuwa marais hao walifikia uamuzi huo baada ya kupokea ripoti maalum kutoka kwa Mkuu wa Majeshi Nchini Kenya Jenerali Robert Kibochi.

Jenerali Kibochi ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Majeshi ya Mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kikosi hicho kitatwikwa wajibu wa kulinda usalama katika mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kaskazini ili “kuleta utulivu kwa ushirikiano na wanajeshi wa DRC”.

Wanajeshi hao pia watashirikiano na kikosi cha Umoja wa Mataifa (UN) kilichotumwa kulinda usalama eneo hilo, maarufu kama MONUSCO.

Wanachama wa kikosi hicho pia wataendesha shughuli ya kuwapokonya silaha waasi wanaoendesha mashambulio katika mikoa hiyo.

Mkutano huo huo wa Nairobi pia uliamuru kusitishwa kwa mapigano katika maeneo hayo na kuondolewa kwa wanajeshi wa mataifa ya DRC na Rwanda wanaopigana katika maeneo ya mipaka ya mataifa hayo mawili.

“Kwa kufanya hivyo, mazingira ya kisiasa yanafaa kuboreshwa na pande zote husika ili kuwaruhusu raia wa DRC kujihisi salama na waweze kuendelea na shughuli zao za kuleta mapato,” taarifa hiyo ikaeleza.

Mkutano huo ulihudhuriwa na marai wafuatao; Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda), Felix Tshisekedi (DRC) na Evariste Ndayishimiye (Burundi).

Mkutano huo wa Marais wa Mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu hali ya usalama DRC ulijiri wakati ambapo kuna uhasama kati ya nchi hiyo na Rwanda.

Hii ni baada ya DRC kuisuta Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 ambalo limekuwa likipigana na wanajeshi wa DRC. Hata hivyo, Rwanda imekana madai hayo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii