Kampuni ya nishati ya Glencore imekiri jana kutoa rushwa ya dola milioni 26.5 kwa mataifa matano ya Afrika katika juhudi zake za kupata mafuta na kutengeneza faida isiyo halali. Ofisi ya makosa makubwa ya udanganyifu ya Uingereza, SFO imesema kampuni hiyo ya Glencore tawi la Uingereza imekiri madai yote ya rushwa dhidi yake mbele ya mahakama ya Southwark Crown. Kampuni hiyo iliipa rushwa Cameroon, Guinea ya Ikweta, Ivory Coast, Nigeria na Sudan Kusini ili kupata upendeleo katika maeneo kadha wa kadha kwenye sekta ya mafuta, ili kujinufaisha. Kesi hiyo ni miongoni mwa msururu wa madai ya hivi karibuni kuhusiana na rushwa yanayoendelea kuchunguzwa kote ulimwenguni.