Serikali yataja sababu risiti za EFD kufutika maandishi

Serikali imetaja sababu za kufutika kwa maandishi  kwenye risiti za mashine ya kodi ya kielektroniki (EFD) kwamba inatokana na kuchapwa kwenye karatasi zisizokuwa na ubora.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatatu Juni 20, 2022 na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,  Hamad Hassan Chande akibainisha kuwa serikali inalifanyia kazi suala hilo.

Naibu waziri huyo ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu,  Angelina Malembeka aliyetaka kujua  mpango wa serikali kuboresha risiti za mashine hizo ili zisifutike baada ya muda mfupi.

“Kufutika huko baada ya muda mfupi kumesababishwa na matumizi ya karatasi zenye ubora hafifu,”amesema Chande.

Amesema baada ya kubaini changamoto hiyo, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana Mamlaka ya Mapato (TRA) imeshatengeneza viwango vya ubora wa karatasi hizo vinavyotakiwa.

Ameeleza kuwa kwa sasa wanaendelea na usimamizi kuhakikisha karatasi zote zinakidhi ubora unaotakiwa.


Kingine ametaja kuwa TRA imeboresha mfumo wa usimamizi wa mashine za EFD kwa kuuwezesha kupokea taarifa zote za kila risiti inayotolewa na kuitunza katika kifaa cha kutunza kumbukumbu na hivyo kuwezesha nakala ya risiti hizo kuweza kupatikana wakati wowote inapohitajika.



Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii