Binti mkubwa wa Rais wa Ufilipino anayeondoka madarakani Rodrigo Duterte ameapishwa kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo.
Sara Duterte ameapa kuwaunganisha Wafilipino katika hafla ya kuapishwa kwake mjini Davao.
Ni katika mji huo ambapo Sara mwenye umri wa miaka 44-alichukua usukani kutoka kwa baba yake kama Meya kwa zaidi yamwongo mmoja uliopita -kabla ya kujitosa katika siasa za kitaifa.
Alikula kiapo kando ya mgombea mwenzake, Ferdinand Marcos Junior, ambaye hivi karibuni atachukua nafasi ya baba yke kama rais.
"Siku zinazokuja zinatarajiwa kuwa na changamoto ambazo zinatuhitaji kuwa na mshikamano kama taifa," Bi Duterte alisema.
Muhula wake wa miaka sita madarakani ukiongozwa na Ferdinand Marcos Junior utaanza rasmi Juni 30.
Kama wangombea katika uchaguzi wa mwezi Mei wawili hao walipata ushindi wa kishindo kwa kubuni muungano thabiti wa kisiasa na kutumia kauli mbiu ya umoja ambao utasaidia baadhi ya washirika wao pia kupata uongozi katika ngazi zingine za serikali.
Nchini Ufilipino , rais na makamu wake wanachaguliwa kando kando.
Bw. Duterte ni mtu mwenye utata ambaye aliingia madarakani mwaka 2016 akiahidi kupunguza uhalifu na kukabiliana na janga la dawa za kulevya.
Lakini wakosoaji wanasema katika kipindi cha miaka mitano madarakani, Bw Duterte alwahimiza polisi kutekeleza maelfu ya mauaji ya kiholela ya washukiwa katika kile alichokiita "vita vyake dhidi ya mihadarati".
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imetaka uchunguzi ufanyike rasmi kuhusu maelfu ya mauaji yaliyotokea wakati wa msako huo mkali.