Raia wa Colombia watampigia kura rais mpya leo Jumapili katika uchaguzi uliojaa sintofahamu. Mwanaharakati wa zamani Gustavo Petro na mfanyabiashara milionea Rodolfo Hernandez wanawania mamlaka katika nchi iliyojaa umaskini mkubwa, ghasia na masaibu mengine. Kunatarajiwa idadi kubwa ya raia watakaosusia uchaguzi huo huku wapiga kura wakikabiliwa na chaguo gumu kati ya kumchagua rais wao wa kwanza kabisa wa mrengo wa kushoto au kumchagua mgombea aliyebatizwa jina la Donald Trump wa Colombia. Kampeni ilikuwa na mvutano mkali na kuna hofu kwamba matokeo ya leo yanaweza kuzusha vurugu za baada ya uchaguzi. Atakayechukua nafasi ya Rais wa kihafidhina Ivan Duque, atalazimika kushughulikia nchi iliyo katika mzozo kutokana na janga la Uviko-19, mdororo wa uchumi, ongezeko la ghasia zinazohusiana na biashara ya dawa za kulevya na hasira kali ya umma dhidi ya taasisi za kisiasa.