Marekani imetangaza kuwa balozi Mike Hammer ndiye atakayehudumu kama mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la Pembe ya Afrika. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amesema katika taarifa yake kwamba mjumbe huyo anachukua nafasi hiyo wakati ambapo eneo la Pembe ya Afrika linakabiliwa na misukosuko ya kisiasa. Blinken amesema mjumbe wa awali, David Satterfield, anajiandaa kuacha wadhifa wake huo. Mjumbe mpya Mike Hammer anasubiriwa na mzozo wa nchini Ethiopia na mizozo ya kiuchumi na kisiasa katika nchi ya Sudan baada ya mapinduzi ya mwezi Oktoba nchini humo. Kwa sasa Hammer ni balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na hapo awali aliwahi kuwa balozi wa Marekani nchini Chile. Amekuwa pia na majukumu mengine mbalimbali katika wizara ya ulinzi na katika ikulu ya Marekani.