WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Innocent
Bashungwa na viongozi wengine wa wizara hiyo wahakikishe kuwa suala la
ukusanyaji mapato kwenye Mikoa, Halmashauri na Mamlaka za Serikali za
Mitaa linapewa kipaumbele ili kuongeza mapato ya Serikali..
“Ajenda
ya ukusanyaji mapato iwe ya kudumu ili yaongezeke hadi kufikia shilingi
trilioni 2 kutoka makadirio ya sasa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo
Halmashauri zimekadiria kukusanya mapato ya ndani ya shilingi trilioni
1.01 ikilinganishwa na shilingi bilioni 863.85 zilizoidhinishwa kwa
mwaka 2021/2022,” amesema.
Ametoa wito huo Mei 31, 2022
alipokutana na Waziri wa TAMISEMI, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Naibu
Makatibu Wakuu pamoja na Wakurugenzi na Wakuu wa taasisi za wizara hiyo
kwenye kikao alichokiitisha jijini Dodoma ili kuwakumbusha wajibu wao.
“Nimekuja
kwenye ziara ya kawaida ya kiutendaji ili kuzungumza na viongozi wakuu
wa wizara na wakuu wa idara. Ni lazima ujitambue wewe ni nani hapa
kwenye wizara, unatakiwa kufanya nini, mpango kazi wako ukoje na je ni
wako peke yako ama unahitaji watu wengine ili uweze kuutekeleza,”
amesema.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona
Watanzania wanafikiwa na huduma. Ni lazima tujiulize, je huduma hizo
zinafika kwa wananchi kwa wakati. Watanzania wanaitegemea TAMISEMI
kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, halmashauri, kata vijiji hadi vitongoji.
Kwa hiyo, tunapaswa kuhakikisha hiyo chain inafanya kazi,” amesema.
Amesema
watumishi hao wanapaswa kutambua kwamba bila uaminifu, uadilifu na
uwajibikaji hawawezi kufanikiwa lakini pia wanapaswa kusimamia mambo
hayo matatu hadi ngazi za chini
Amewapongeza viongozi na
Watendaji wa wizara kwa kufanikiwa kuongeza hati safi kwenye taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) katika kipindi cha mwaka
2019/2020 na 2020/2021.
“Taarifa ya CAG kuhusu Hesabu za Mamlaka
za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imebainisha
Halmashauri 178 sawa na asilimia 96 zimepata hati safi, Halmashauri sita
sawa na asilimia tatu zimepata hati zenye shaka na Halmashauri moja
sawa na asilimia moja imepata hati mbaya”.
Waziri Mkuu amesema
matokeo ya ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2020/2021 yanaonesha
mwenendo mzuri wa aina ya hati za ukaguzi zilizotolewa ikilinganishwa na
ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha wa 2019/2020 ambapo Halmashauri
zilizopata hati safi zilikuwa 124 sawa na asilimia 67, Halmashauri
zilizopata hati zenye shaka zilikuwa 52 sawa na asilimia 29 na
Halmashauri zilizopata hati mbaya zilikuwa nane sawa na asilimia nne.
“Mwaka
huu hati mbaya zimepungua kutoka nane hadi moja, kwa hiyo kama leo
tumefikia asimilia 96 tuna uwezo wa kufikia asilimia 100, kutafuta ile
mbaya na zenye mashaka sita zikaondoka.”
Ameitaka menejimenti ya
wizara hiyo iwe na ubunifu, iongeze matumizi ya TEHAMA ili kuongeza
mapato ya Serikali, Wakuu wa Idara wagawe majukumu kwa wasadizi wao na
wakurugenzi wawe na vikao vya mara kwa mara na wasaidizi wao.