Baadhi
ya washiriki wa Semina kuhusu Sensa ya Watu na Makazi kwa Wabunge
wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua Semina
hiyo kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni jijini Dodoma, Mei 30,2022.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wabunge wawaelimishe na wawahamasishe
wananchi wajitokeza na washiriki katika Sensa ya Watu na Makazi ikiwa ni
pamoja na kutoa taarifa na takwimu sahihi kwa makarani wa Sensa.
Akizungumza
wakati alipofungua Semina ya Wabunge kuhusu Sensa ya Watu na Makazi
kwenye ukumbi wa Msekwa jijini Dodoma leo Mei 30, 2022, Mheshimiwa
Majaliwa amesema kazi ya kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi inapaswa
kufanywa na kila mdau wakiwemo Wabunge ambao wajibu wao ni kuwahudumia
wananchi.
Mheshimiwa
Majaliwa amesema ni muhimu kwa wabunge kushiriki kikamilifu ili kupata
taarifa na takwimu sahihi za idadi ya watu, hali zao za makazi, taarifa
za majengo yote nchini hatua ambayo itawawezeshe kuwatumikia vyema
wananchi.
“Tunapenda
kuona kila Mheshimiwa Mbunge anaona fahari kuwa watu wote katika jimbo
lake wamehesabiwa na wametoa taarifa na takwimu sahihi zinazoakisi idadi
halisi ya watu na makazi yao katika eneo husika.”
Amesema
Tanzania ni moja kati ya nchi chache Barani Afrika ambazo zimeweza
kufanya Sensa katika vipindi vyote vya utekelezaji wa Mipango Mikakati
ya Umoja wa Mataifa wa Kufanya Sensa.
“Ninapenda
kuwaarifu Waheshimiwa Wabunge kuwa maandalizi ya sensa yanaendelea
vizuri na sasa tumefikia zaidi ya asilimia 80. Napenda kuwahakikishia
kuwa Serikali imejipanga vyema kuhakikisha kuwa Sensa inafanyika kama
ilivyopangwa ikiwa ni pamoja na kutoa matokeo bora kulingana na viwango
vya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa wakati,” alisisitiza Mheshimiwa
Majaliwa .
Akimkaribisha
Waziri Mkuu kufungua Semina hiyo, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson
Mwansasu amewashukuru makamisaa na watalaamu wa Sensa kwa semina na
mafunzo mbalimbali ambayo wamekuwa wakiwapatia wabunge kwa nyakati na
makundi tofauti.
Amesema
wabunge wanalichukulia suala la kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu
wa kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi na kutoa taarifa
sahihi kwa Makarani kuwa ni la msingi.
Mheshimiwa
Tulia amesema Bunge litatamani kuona kwamba zoezi la sensa na Makazi
ya Watu linaenda vizuri ili takwimu sahihi zitazopatikana ziwasaidie
wabunge kuishauri Serikali kupanga na kugharimia shughuli za maendeleo
nchini kwa kuzingatia idadi ya watu katika eneo husika.
Naye,
Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu Anne Makinda amesema anashukuru kuona
kwamba makundi yote waliyokutana nayo yameonesha nia na dhamira ya
kutoa ushirikiano ili kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi wakiwemo
Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilsihi.
Kauli
mbiu ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23
mwaka huu ni ‘Sensa kwa Maendeleo Jitokeze Kuhesabiwa’.
Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii