Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amesema serikali yake itapeleka muswada bungeni kuweka zuio la nchi nzima kwa watu kumiliki bastola pamoja na kupiga marufuku raia wa Canada kuuza au kununua bastola kokote nchini humo. Iwapo muswada huo utaidhinishwa marufuku ya kumiliki bastola itaanza kutekelezwa wakati wa majira ya mapukutiko. Trudeau amewaambia waandishi habari kuwa muswada huo pia unapendekeza kuwapokonya silaha watu wote waliotiwa hatiani kwa matendo ya unyanyasaji majumbani. Kadhalika serikali itaweka zuio kwenye mauzo ya risasi ambapo watu wenye bunduki hawataruhusiwa kununua kasha lenye zaidi ya risasi tano kwa wakati mmoja. Mauaji ya wanafunzi 19 na walimu wawili yaliyotokea nchini Marekani wiki iliyopita yamechochea mjadala kuhusu umuhimu wa kudhibiti umiliki wa silaha kote duniani. Canada ambayo tayari ina sheria kali za kumiliki bunduki inalenga kuongeza makali ya masharti hayo.