HALI YAWA TETE KWA GAMBO, WANNE WAHOJIWA.

Tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma zilizoibuliwa wiki iliyopita Jijini Arusha na kusababisha watumishi sita kusimamishwa kazi, zinazidi kulitikisa Jiji hilo baada ya idadi ya wanaohusishwa nazo kufikia wanane.

Wiki iliyopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwasimamisha kazi watumishi hao wa Halmashauri ya Jiji la Arusha akiwamo Mkurugenzi wake Dk John Pima kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha na kulikabidhi suala hilo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili ichunguze.

Katika sakata hilo, Mbunge wa Arusha mjini (CCM), Mrisho Gambo alimtaja Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM)Taifa, Kenan Kihongosi kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Hata hivyo, jana Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, James Ruge aliliambia gazeti hili kuwa idadi ya wanaohojiwa na taasisi hiyo imeongezeka kutoka sita wa awali hadi nane kutokana na kubaini kuwepo kwenye mnyororo wa tuhuma hizo.

“Ukiachilia mbali wale watuhumiwa sita tuliokabidhiwa, lakini sasa tumeongeza wengine wawili ambao katika uchunguzi wetu tumeona tuwahoji hivyo watuhumiwa wamefikia wanane lakini wengine wengi watafuata,”alisema Ruge.

Hata hivyo Kamanda Ruge hakuwa tayari kuwataja watuhumiwa hao kwa kuwa bado wanaendelea na uchunguzi ambao wamebaini kuwepo kwa mnyororo mrefu lakini kwa kuwa kazi hiyo wanaifaya kwa kushirikiana na taasisi nyingi ikiwemo benki.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii