Mchakato wa kuuzwa kwa Chelsea unakamilika rasmi leo Mei 30, 2022

MCHAKATO wa kuuzwa kwa Chelsea unakamilika rasmi leo Jumatatu, Mei 30, 2022 baada ya maelewano ya “mwisho na dhahiri” kuafikiwa na kampuni inayoongozwa na  Todd Boehly.

Serikali ya Uingereza na vinara wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wameidhinisha mpango wa kuuzwa kwa Chelsea kwa pauni 4.25 bilioni.

Chelsea ilitiwa mnadani mnamo Machi 2022 baada ya aliyekuwa mmiliki wake, bwanyenye Roman Abramovich, kuwekewa vikwazo kwa madai ya kuwa na uhusiano wa karibu na rais wa Urusi, Vladimir Putin, aliyeongoza uvamizi dhidi ya Ukraine.

Klabu hiyo imekuwa ikiendesha shughuli zake kwa leseni spesheli itakayokatika rasmi mnamo Mei 31.

“Klabu ya soka ya Chelsea inathibitisha kwamba makubaliano ya mwisho, dhahiri na madhubuti yamefanywa kuhusu kuuzwa kwa kikosi hiki kwa muungano wa Todd Boehly/Clearlake Capital,” ikasema sehemu ya taarifa ya Chelsea mnamo Mei 28, 2022.

Abramovich aliyenunua Chelsea mnamo 2003 kwa pauni 140 milioni, amesema “ameridhishwa na kufurahishwa na hatua ya kukamilika vyema kwa shughuli ya kutafutwa kwa mmiliki mpya wa Chelsea.”

Chelsea walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2021-22 katika nafasi ya tatu huku wakipoteza fainali za Carabo Cup na Kombe la FA dhidi ya Liverpool kwa penalti. Walidenguliwa na Real Madrid ya Uhispania kwenye hatua ya robo-fainali.

Chini ya Abramovich, Chelsea walishinda mataji mawili ya UEFA, matano ya EPL, matano ya Kombe la FA, mawili ya Europa League na matatu ya Carabao Cup.

Mnamo Agosti 2021, walishinda Uefa Super Cup kabla ya kunyanyua Kombe la Dunia mnamo Februari 2022. Abramovich ameteua makocha 13 tofauti huku kikosi hicho kikimwaga sokoni kima cha pauni 2 bilioni kwa ajili ya usajili wa wanasoka wapya.

Timu ya wanawake ya Chelsea iliyoanza kuwa sehemu ya klabu ya wanaume mnamo 2004 nayo imeshinda mataji manne ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini Uingereza (WSL) na matatu ya Kombe la FA chini ya Abramovich.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii