Serikali mbioni kuvifungulia vyombo vya habari

Serikali imesema ipo mbioni kuvifungulia vyombo vya habari ambavyo bado vimefungiwa mara baada ya kumaliza mazungumzo yanayoendelea hivi sasa baina ya mamlaka na wahusika.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne, Desemba 7, 2021 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju wakati akizindua kikao kazi cha Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) kinachofanya marejeo na kuchambua mapendekezo 252 ya haki za binadamu.

Mpanju amesema lengo la Rais Samia ni kuhakikisha anarejesha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Hili ni miongoni mwa mapendekezo mliyoyatoa, itakapofika Februari 14 tutasimama na kutaja mapendekezo ambayo Serikali itakuwa imeyakubali na mpaka sasa tayari mengi yameshafanyiwa kazi likiwamo la  wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni.

“Uhuru wa vyombo vya habari ni jambo ambalo Rais Samia Suluhu Hassan amelisimamia na anahitaji matokeo ya haraka. Tumeshakutana na wadau na jana tumekutana na mamlaka husika kupitia vifungu vyote kuhakikisha kwamba tunavifungulia vyombo vyote vya habari ambavyo vilifungiwa. Rais ameagiza lazima tumalize hili jambo,” amesema Mpanju.

Awali Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema Serikali ni muhimu ikubali mapendekezo ya kuondoa sheria ambazo zinaminya uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza.

Amesema pia muhimu kukubaliwa mapendekezo ya  kuzifanyia maboresho sheria zilizofungia magazeti,sheria ya makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 , Sheria ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 2016 na kuruhusu watoto wakipewa ujauzito kurejea shule.

Hata hivyo amesema ingawa kuna mapendekezo hayakukubaliwa katika kikao cha mapitio ya utekelezaji wa Haki za Binaadamu (UPR) lakini baadhi tayari yameanza kufanyiwa kazi ikiwapo kurejeshwa kwa wanafunzi shule waliopata ujauzito

Mpaka sasa Tanzania imekubali asilimia 43 ya mapendekezo ya haki za binadamu katika mchakato wa mapitio ya hali ya haki za binadamu.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii