Rais Samia aahidi sapoti zaidi kwa Tembo Warriors

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya taifa ya soka ya Walemavu ‘Tembo Warriors’ kwa kufuzu kuiwakilisha nchi kwenye kombe la dunia.

Rais Samia ameipongeza timu hiyo katika hafla iliyofanyika leo Ikulu, Dar es Salaam na kusisitiza kuwa Tembo Warriors imeonyesha mfano.

Amesema pamoja na kwamba imeanzishwa miaka ya hivi karibuni, lakini imeandika rekodi hiyo huku akibainisha kuendelea kuisapoti na kutaka ifanye maandalizi bora kuelekea kwenye mashindano hayo ya Oktoba 2022 nchini Uturuki.

"Kombe la dunia ni kombe la dunia, liwe la bao, kucheza karata au vinginevyo, ni kombe la dunia, wanangu hawa wanahitaji pongezi," amesema Rais na kuongeza.

"Tembo Warriors imeanzishwa mwaka 2018, lakini kuna timu zimeundwa tangu wengine hamjazaliwa lakini hazijawahi kufuzu, tunazisikia tu mara kasajiliwa huyu mara yule, ila wanangu hawa wamefuzu," amesema.

Amesema anaona kishindo cha Tembo Warriors kitakavyokuwa kwenye mashindano ya dunia na kubainisha kwamba ili kufanya vizuri ni maandalizi.

"Tukiwatawanya sasa tutawavuta mwakani Juni au vinginevyo, kuwaunganisha tena, itakuwa ni kazi hivyo Serikali itafikiria jinsi ya kufanya lakini pia nitawapangia mlezi ambaye atawalea vema kwa kuwa Rais ana mambo mengi," amesema.

Awali rais wa Shirikisho la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu, Peter Sarungi na waziri wa Michezo, Innocent Bashungwa walimshukuru Rais kwa sapoti aliyoionyesha kwenye timu hiyo wakati wa maandalizi hadi kwenye mashindano ya Afrika ambayo Tanzania ilikuwa mwenyeji huku Sarungi akimuomba Rais Samia kuwa mlezi wa timu.

"Rais ana mambo mengi, ila nitawapangia mlezi ambaye atawalea vizuri," amesema Rais Samia akijibu ombi la Sarungi.

Aidha Rais Samia amempongeza Frank Ngailo ‘Mbappe’ kwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo aliyepachikwa jina la Mbappe.

Tembo Warriors itashiriki kombe la dunia kwa mara ya kwanza huku ikiwa na rekodi ya kushiriki mara mbili mashindano ya Afrika ambayo msimu huu yalifanyika kwa muhula wa sita na Tanzania ikiwa mwenyeji.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii