Biden aunga mkono kuanzishwa upya mazungumzo kati ya Maduro na upinzani

Rais wa Marekani Joe Biden amezungumza kwa njia ya simu na kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan Guaido na kueleza uungaji mkono wa Marekani wa kuanzishwa upya mazungumzo kati ya serikali ya Rais Nicolas Maduro na upinzani. Akizungumza kutoka ndege aina ya Air Force One akiwa njiani kuelekea mkutano wa kilele wa viongozi wa mabara ya Amerika unaofanyika mjini Los Angeles, Biden amesisitiza kuwa Washington iko tayari "kulegeza vikwazo" dhidi ya Venezuela kwa kutegemea matokeo ya mazungumzo kati ya serikali na upinzani. Maduro ambaye hakualikwa kwenye mkutano huo, hata hivyo bado hajaweka wazi tarehe maalum ya kuanza tena kwa mazungumzo hayo. Marekani inamtambua Guaido kama rais wa mpito baada ya kukataa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2018 yaliyomrudisha tena Maduro madarakani ikidai uchaguzi huo ulikumbwa na dosari nyingi. Hata hivyo, kiongozi huyo wa kisoshalisti bado amesalia madarakani katika nchi hiyo mwanachama wa jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani Opec, licha ya vikwazo vikali vya Marekani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii