Wagonjwa 1000 wakutwa na homa ya nyani katika nchi 29 ikiwemo Ulaya

Shirika la afya duniani WHO limetahadharisha juu ya hatari ya kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nyani hasa katika mataifa ya Ulaya, huku kukiwa na zaidi ya watu 1,000 waliokutwa na homa hiyo katika nchi ambazo awali hazikuwahi kuripoti ugonjwa huo. Mkuu wa shirika hilo la Umoja wa mataifa Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema shirika hilo halipendekezi kutolewa kwa chanjo ya watu wengi dhidi ya ugonjwa huo kwa wakati huu. Ameeleza pia hakuna vifo vyovyote vilivyotokea hadi sasa kutokana na homa hiyo ya nyani. Awali ugonjwa huo uliripotiwa katika nchi tisa za Afrika japo katika miezi ya hivi karibuni, umeenea katika mataifa kadhaa ya Ulaya hasa Uingereza, Uhispania na Ureno. Ugiriki imekuwa nchi ya hivi karibuni kabisa kuthibitisha mgonjwa wa kwanza wa homa ya nyani, huku mamlaka nchini humo ikisema mgonjwa huyo ni mwanamume ambaye hivi majuzi alisafiri hadi Ureno. Dalili za awali za homa hiyo zinatajwa kuwa ni homa kali, vipele vinavyoweza kuwa na usaha au majimaji, vipele vya malengelenge kwenye ngozi kama vile tetekuwanga.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii