Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimewasilisha azimio kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati IAEA na kuikosoa vikali Iran kwa kutoshirikiana na shirika hilo. Katika azimio hilo ambalo ni kwanza tangu Juni mwaka 2020 wakati azimio sawa na hilo lilipopitishwa, mataifa hayo yenye nguvu kubwa duniani yameitaka Iran kushirikiana kikamilifu na IAEA. Katika taarifa ya pamoja kwa bodi ya magavana wa shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati inayokutana wiki hii, Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimesema zinaitaka Iran kuacha kabisa kuendelea na mipango yake ya nyuklia na badala yake kukumbatia mkataba kati ya Tehran na mataifa yenye nguvu duniani. Azimio hilo ni ishara ya kupungua kwa subra kutoka nchi za magharibi baada ya mazungumzo ya kufufua makubaliano ya kihistoria ya nyuklia ya mwaka 2015 kukwama mwezi Machi. Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya IAEA, Jamhuri hiyo ya Kiislamu ina kilo 43.1 za madini ya Urani yaliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 60 japo Iran inakanusha kuwa inataka kutengeneza silaha za nyuklia.