Ashraf Ghani hakuimbia Afghanistan na mamilioni ya pesa

Ripoti ya shirika la Marekani linalofuatilia jinsi mabilioni ya dola yanavyotumiwa na Marekani kwa ujenzi mpya wa Afghanistan SIGAR imesema rais wa zamani wa Afghanistan Ashraf Ghani hakuikimbia nchi hiyo akiwa na mamilioni ya pesa zilizoibwa. Ripoti hiyo ya SIGAR ambayo itachapishwa leo Jumanne, ni stakabadhi ya muda tu, wakati ofisi inasubiri majibu ya maswali yaliyotumwa kwa rais huyo wa zamani wa Afghanistan kuhusu suala hilo. Waandishi wa ripoti hiyo kwanza waliwahoji mashahidi na maafisa waliokuwa kwenye msafara wa helikopta na Ghani wakati walipokuwa wanatoroka kutoka ikulu ya rais mjini Kabul baada ya Taliban kuchukua udhibiti wa mji mkuu Agosti 15. Ripoti za awali zilidai kuwa Ghani na maafisa wengine walichukua hadi dola milioni 169 kutoka hazina ya serikali japo rais huyo wa zamani amekanusha vikali madai hayo. Ripoti hiyo ya SIGAR inaendelea kueleza kuwa, imegundua fedha zilichukuliwa kutoka hazina ya serikali na kupakiwa kwenye helikopta lakini ushahidi unaonyesha kiwango hicho cha pesa hakikuzidi dola milioni moja. Shirika hilo la uangalizi la Marekani hata hivyo limesema halina ushahidi wa kutosha kuthibitisha iwapo fedha nyengine ziliibiwa na maafisa wengine wa Afghanistan wakati serikali iliyotambulika kimataifa ilipoanguka.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii