Kura ya kutokuwa na imani dhidi ya Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson imeshindwa kufaulu katika bunge la Uingereza lakini idadi kubwa ya wabunge katika chama chake cha kihafidhina walipiga kura ya "ndio" kuunga mkono kuondolewa kwake madarakani. Uasi katika chama chake juu ya kashfa ya "partygate", unaonekana kuwa pigo kwa mamlaka yake na kumwacha Waziri Mkuu huyo katika hali ngumu ya kutafuta uungwaji mkono upya. Johnson ambaye alipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2019, amekuwa chini ya shinikizo kubwa baada ya kuandaa sherehe ya unywaji pombe katika ofisi yake ya Downing Street na makaazi yake wakati Uingereza ilipokuwa chini ya vizuizi vikali vya Corona. Katika siku za hivi karibuni, Johnson alizomewa na umma wakati wa hafla za kusherehekea maadhimisho ya miaka 70 ya uongozi wa Malkia Elizabeth inayojulikana kama Jubilee ya Platinum.