Namungo, Aussems sasa wanayajenga

NAMUNGO ni miongoni mwa timu inayopitia wakati mgumu kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na kushindwa kupata matokeo mazuri huku ikielezwa kuwa matokeo haya yamepelekea viongozi kuanza kusaka kocha mpya.

Namungo chini ya kocha Hemed Morocco inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa imekusanya pointi 6, imeshinda mechi moja, sare tatu na imepoteza mechi tatu.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema kuwa viongozi wameanza kufanya mazungumzo na aliyekuwa kocha wa Simba na sasa anaifundisha AFC Leopards ya Kenya, Patrick Aussems kuona namna gani watampata.

“Namungo wamemtumia hadi mikataba yao Aussems na wamefanya mazungumzo kwa ukaribu na kocha huyo, kinachosubiriwa ni maamuzi ya pande zote mbili kulingana na hali ilivyo,” kilisema chanzo chetu na kuongeza;

“Aussems bado ana mkataba na Leopards ili kumtoa hapo lazima kuna kiasi fulani cha pesa kinatakiwa kulipwa na wao ndio waweze kumuachia hivyo Namungo kazi ipo kwao,”

“Kama Namungo watafanya hilo na wakakubaliana na Aussems litakuwa suala hili limemalizika na atakuja nchini kwani mwenyewe yupo tayari kurudi Tanzania kufundisha soka.”

Kwa upande wa Aussems alisema mbele yake kuna ofa za timu nyingi hapa Afrika ambazo zimeonyesha nia ya kumuhitaji ila ameshindwa kufanya maamuzi kwani bado yupo na sehemu ya mkataba wa Leopard.

“Kama kuna timu ambayo inaweza kuelewana na waajiri wangu pamoja na yale matakwa yangu sina sababu au kuzuizi cha aina yoyote kushindwa kujiunga nao,” alisema Aussems na kuongeza;

“Katika mpira lolote linaweza kutokea kwa wakati huu tusubiri na tuone jambo gani litakuja mbele yangu kama nitabaki hapa au kuondoka mahala pengine.

“Awali kulikuwa na suala hilo la Azam niliwahi kuzungumza na kiongozi mmoja wa juu wa timu hiyo lakini tangu hapo hakuna lolote ambalo liliendelea baada ya hapo.”

Katibu wa Namungo, Ally Suleiman alisema wanachosubiri ni uongozi wa juu ufanye maamuzi.

“Hakuna lolote ambalo nalifahamu kuhusiana na suala la kocha ila Uongozi wa juu wao ndio wenye maamuzi,” alisema Suleiman.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii