Serikali imesema kuwa inaendelea kulishughulikia sauala la migogoro ya watu wa Mindu mkoani Morogoro hivyo wananchi wake wasiwe na wasiwasi.
Kauli hiyo iletolewa leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la papo kwa hapo la mbunge wa Morogoro Abdulazizi Aboud.
Mbunge huyo amehoji kuhusu upimaji wa ardhi kwenye maeneo yenye migogoro na yanayotajwa kuwa ni vyanzo vya maji ambako baadhi ya wananchi wako mbali lakini wanatakiwa kuondoka.
Aboud amesema jambo hilo limekuwa likitoa taharuki kubwa kwa baadhi ya wananchi kwenye maeneo hayo hivyo akaomba Serikali kutoa tamko la kuwaondolea hofu wananchi.
Waziri Mkuu amesema migogoro ya wananchi wa Mindu katika mkoa wa Morogoro imekuwa ya siku nyingi na kwamba mara kadhaa wamekwenda kwake na mbunge.
“Naufahamu mgogoro huu, mara kadhaa mbunge huyu amekuja na wananchi wake kuhusu migogoro hiyo, naomba wananchi wavute subira ili tuendelee kulitazama na tutakapoona inafaa kuwaleta mawaziri 8 tutaleta kwako kumaliza jambo hilo,” amesema Waziri Mkuu.
Akijibu swali la mbunge wa Mbarali, Francis Mtega kuhusu baadhi ya maeneo ambayo hayajapitiwa na timu ya mawaziri nane licha ya kuwa na migogoro, alisema kazi inaendelea.
Mtega alihoji ni lini timu hiyo itapitia maeneo ambayo hawakupitia wakati kuna migogoro mikubwa ya ardhi.
Waziri Mkuu amesema timu ya mawaziri nane imeendeela kufanya kazi kwa maeneo yote yenye migogoro ilianza kufanya kazi mwaka 2019 na tayari ilishapeleka bungeni kuhusu vijiji vilivyopitiwa.
Amesema migogoro mingi inamalizwa na ngazi ya viongozi ya vijiji na ngazi zingine lakini, matatizo makubwa ndiyo yanashughulikiwa na timu ya mawaziri nane ambayo inatarajia kukamilisha kazi yake muda mchache na kupeleka taarifa bungeni.