Kim awalaumu maafisa wa serikali yake kuenea kwa corona

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un amewalaumu maafisa wa serikali yake kwa uzembe uliosababisha hali ya janga la virusi vya corona nchini humo kuwa mbaya zaidi. Haya yameripotiwa na shirika la habari la taifa nchini humo KCNA, wakati ambapo idadi ya walioambukizwa ikiwa imepindukia watu milioni 1.7. Katika mkutano na maafisa wa chama tawala Politburo hapo jana, Kim aliahidi kuwachangamsha maafisa hao ili wakabiliane vilivyo na kusambaa kwa virusi hivyo. Kim amejiweka mstari wa mbele katika mapambano ya virusi hivyo Korea Kaskazini akisema kuenea kwake kunasababisha malalamiko mengi nchini humo. Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amewaambia waandishi wa habari kwamba ana wasiwasi mkubwa kuhusiana na hatari ya kuenea zaidi kwa virusi hivyo Korea Kaskazini kwa kuwa idadi kubwa ya raia hawajachanjwa na wana magonjwa mengine yanayowaweka hatarini endapo wataambukizwa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii