Mawaziri Uhispania wapitisha likizo ya wanawake walio katika hedhi

Baraza la mawaziri la Uhispania limeidhinisha mswada unaowapa wanawake likizo ya kimatibabu yenye malipo, wanapopitia maumivu makali kipindi cha hedhi. Uhispania sasa inakuwa nchi ya kwanza ya Ulaya kupitisha sheria kama hiyo. Lakini mswada huo ni sharti uidhinishwe na bunge la nchi hiyo huku ukitarajiwa kupigiwa kura katika miezi michache ijayo. Haijabainika wazi iwapo serikali ya muungano ya Kisoshalisti yake Waziri Mkuu Pedro Sanchez ambayo imetoa kipaumbele kwa haki za wanawake kama ina uungwaji mkono kikamilifu bungeni kuupitisha mswada huo na kuwa sheria. Waziri anayeshughulika na masuala ya usawa wa Uhispania, Irene Montero amesema sheria hiyo itatambua tatizo la kiafya ambalo kwa muda mrefu limekuwa likipuuzwa. Kwa sasa wanawake walio katika hedhi wanapewa likizo katika nchi chache tu duniani zikiwemo Korea Kusini na Indonesia.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii