Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametangaza
kuondolewa kazini Wakurugenzi watano wa Bohari ya Dawa (MSD), kufuatilia
malalamiko mengi ambayo yamekuwa yakitolewa na wabunge na wadau wengine
kuhusu utendaji usioridhisha wa bohari hiyo.
Waziri Ummy Mwalimu
ameliambia bunge jijini Dodoma kuwa pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan
kubadilisha uongozi wa juu wa MSD na kumteua mwenyekiti mpya wa bodi,
hatua hiyo ilikuwa haitoshi kutokana na malalamiko mengi yaliyokuwa
yakitolewa.
“Mkurugenzi wa Fedha anaondoka MSD, Mkurugenzi wa
manunuzi MSD, Mkurugenzi wa Logistics MSD, Mkurugenzi wa Sheria MSD na
Mkurugenzi wa Utawala wa MSD anaondoka.” amesema Waziri Ummy Mwalimu
Waziri
huyo wa Afya ametangaza uamuzi huo wakati akihitimisha mjadala wa
bajeti kwa wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, baada ya
kuchangiwa na wabunge mbalimbali.
Pia amesema wizara ya afya
itasimamia ubora na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na kuipima MSD kwa
upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa miezi mitatu mitatu badala ya
mwezi mmoja mmoja