Kimeumana! Sauti Sol Kushtaki Azimio la Umoja kwa Kutumia Wimbo wao Kuzindua Mgombea Mwenza Martha Karua.

Kundi la wanamuziki la Sauti Sol limetishia kushtaki muungano wa Azimio la Umoja kwa kutumia wimbo wao wa Extravaganza bila idhini yao.
Katika taarifa iliyotiwa sahihi na wanamuziki wanne wa kundi hilo, Sauti Sol inatuhumu muungano huo unaaongozwa na Raila Odinga kwa kukiuka sheria za hakimiliki.

“Imetufikia kuwa Azimio la Umoja kupitia kwa mgombea wao wa urais Raila Odinga kwa mitandao ya kijamii (Twitter, Facebook na Instagram) bila leseni wala mamlaka ulitumia moja wa nyimbo zetu maarufu Extravaganza katika uzinduzi wa mgombea mwenza,” Sauti Sol walisema.
Kwa mujibu wa kundi hilo, muungano huo haukuwa na idhini ya kutumia wimbo wao katika uzinduzi wa mgombea mwenza na hivyo ulikiuka sheria za Kenya kuhusu hakimiliki.
“Hatukupeana leseni ya wimbo huu kwa kampeni za Azimio la Umoja wala hatukuwapa idhini ya kuutumia katika kutangaza mgombea mwenza. Hatua hii ni upuuzaji wa kimaksudi wa haki za msingi za umiliki na uhuru wa kutangamana,” taarifa hiyo iliongeza.


Kundi hilo limejitangaza kama lisiloegemea upande wowote wa kisiasa na kusisitiza kuwa litaelekea mahakamani kudai haki.
“Tumekasirishwa na hatua ya kampeni ya Azimio la Umoja kupuuza haki yetu ya kudhibiti matumizi ya hakimilika. Tutakuwa tukitafuta msaada wa sheria kwa kuwa huu ni ukiukaji wa wazi wa hakimiliki,” taarifa hiyo ilihitimisha.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii