Korea Kaskazini yaripoti vifo 15 zaidi kutokana na 'homa'

Korea Kaskazini leo imeripoti vifo 15 zaidi kutokana na kile ilichokiita homa, siku chache baada ya kuthibitisha rasmi maambukizo yake ya kwanza kabisa ya virusi vya corona na kuagiza vizuizi vikali vya kitaifa vya kuzuia kuenea kwa maambukizo hayo.Mripuko huo ambao kiongozi wa taifa hilo Kim Jong Un amesema unasababisha utata mkubwa, unaiacha nchi hiyo iliyo na mifumo duni zaidi ya afya katika hatari ya uwezekano wa kuzuka kwa janga. Korea Kaskazini haina chanjo za virusi vya corona, dawa za kutibu virusi hivyo au uwezo wa kupima watu kwa wingi. Licha ya kuanzisha mfumo wa juu wa karantini ya dharura ili kupunguza kasi ya kuenea kwa maambukizo hayo, taifa hilo sasa linaripoti idadi kubwa ya visa vya maambukizo mapya kila siku. Shirika la habari la serikali KCNA, leo limeripoti kuwa watu 42 wamefariki tangu kuzuka kwa mripuko huo huku kukiwa na visa zaidi ya laki nane na takriban watu laki tatu wakipokea matibabu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii