Urusi imesema leo kuwa inatafanya mipango ya kuongeza uzalishaji wake wa nafaka kwa ajili ya kuuza nje katika msimu ujao. Hii ni wakati kukiwa na mzozo wa chakula ulimwenguni uliozidishwa na uvamizi wa kijeshi wa Moscow nchini Ukraine. Hatua hiyo ya kijeshi na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi kuhusu uvamizi huo vimeathiri uuzaji wa kimataifa wa nafaka, ngano na bidhaa nyingine. Urusi na Ukraine pekee huzalisha asilimia 30 ya ngano inayouzwa ulimwenguni. Waziri wa Kilimo wa Urusi Dmitry Patrushev amesema katika msimu wa sasa wa mwaka wa 2021-2022 nchi hiyo imeuza nje zaidi ya tani milioni 35 za nafaka, zikiwemo tani milioni 28.5 za ngano. Amesema katika msimu ujao kuanzia Julai mosi mwaka huu, wanakadiria kuuza karibu tani milionio 50 za ngano. Nchi za Magharibi zinaituhumu Kremlin kwa kutumia bidhaa za chakula kama silaha wakati huu wa operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine na kwa kuiba nafaka ya Ukraine kutoka maeneo yanayodhibitiwa na Urusi. Urusi inakanusha madai hayo, ikisema inaweza kuweka maeneo salama nchini Ukraine ya kusafirisha bidhaa, na kusaidia kuepusha mzozo wa chakula duniani, kama vikwazo vya kimataifa ilivyowekewa Urusi vitaondolewa.