Saido ndiyo basi tena

YANGA wamepania kwa namna yoyote ile kushinda mechi ya Jumamosi dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza na hawataki masihara kwenye jambo lao.

Habari za uhakika zimethibitisha kwamba wameweka ulinzi wa kimafia kambini mjini Shinyanga na ni mwendo wa mtu na mtu.

Mtego huo umewanasa mastaa wawili, Saido Ntibazonkiza na Dickson Ambundo baada ya kutoka nje ya kambi kinyume na utaratibu na hata walipoambiwa wakalazimisha yakawakuta yaliyowakuta ambayo yanakwenda kufunga faili la Yanga na Saido.

Yanga ambao hawataki kuona pilika zozote kambini au maeneo yanayozunguka hoteli yao au uwanja wa mazoezi, wanatumia wanachama, mashabiki na viongozi waandamizi kutekeleza hilo.

Saido na Ambundo jana waliondolewa kambini na Kocha Nabi baada ya kudaiwa kutoka kambini juzi usiku bila taarifa zozote na hata walipoambiwa inadaiwa kwamba walikuwa watata.

Licha ya kwamba haijafahamika maramoja kwamba walitoka nje ya kambi kufuata nini lakini vigogo wa Yanga na Nabi wamewatoa wakidai kwamba chochote walichokwenda kufanya ni kinyume.

Yanga ambao wamepania kushinda mechi hiyo, inadaiwa kwamba imefanya uamuzi pia wa kuchana na Saido moja kwa moja kwani hata mkataba mpya alikuwa anazingua kusaini. Habari zinasema kwamba Saido ameshawaaga rasmi viongozi.

Chanzo chetu cha kuaminika kilipasha kwamba wachezaji hao usiku wa juzi walitoka kambini usiku baada ya sare ya 1-1 na Biashara United na Nabi aliwaamuru wasirudi tena.

Saido baada ya kurudi Dar es Salaam alikusanya kilicho chake na kuondoka kwenda Burundi kujiunga na timu yake ya Taifa inayocheza na Cameroon Mei 5, Dar.

Ambundo ambaye amebakiza msimu mmoja, hajarudi Dar es Salaam amesalia kwao Mwanza.

Viongozi wa juu wa Yanga jana walikwepa kuzungumzia sakata hilo kwa maelezo kwamba wako bize na mechi ya Jumamosi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii