Zaidi ya watu 200 wagundulika kuambukizwa virusi vya homa ya kima ulimwenguni - ECDC

Idadi ya watu waliogunduliwa kuwa na maambukizo ya homa ya kima imefikia 219 nje ya nchi ambako ugonjwa huo ni janga, kwa mujibu wa taarifa ya karibuni kabisa kutoka Kituo cha Udhibiti wa Maradhi cha Umoja wa Ulaya, ECDC. Zaidi ya nchi kumi ambako homa ya kima si jambo la kawaida, hasa barani Ulaya, zimeripoti kuwa na angalau mgonjwa mmoja aliyethibitika kuambukizwa virusi hivyo. Shirika hilo limesema wengi kati ya waliogunduliwa kuwa na ugonjwa huo ni vijana wa kiume wanaojitambulisha kama wapenzi wa jinsia moja. Uingereza, ambako mgonjwa wa kwanza aligundulika mapema mwezi huu, hiiv sasa imethibitisha kuwa na wagonjwa 71. Inafuatiwa na Uhispania yenye wagonjwa 51 na Ureno yenye wagonjwa 37. Nje ya Ulaya, Canada imethibitisha kuwa na wagonjwa 15 na Marekani yenye wagonjwa tisa. Idadi hii iliyoripotiwa usiku wa kuamkia leo ni mara tano zaidi ya ile iliyotolea Mei 20, wakati kituo cha ECDC kilipoanza kuchapisha hesabu ya wagonjwa wa homa hiyo ya kima.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii