Uturuki imerejelea msimamo wake kwamba haitaziruhusu Finnland na Sweden kuwa wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO hadi pale masharti yake kwa mataifa hayo yatakapotimizwa. Baada ya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa nchi hizo mbili za Nord, msemaji na msaidizi mkuu wa Rais Tayyip Erdogan, Ibrahim Kalin amewaambia waandishi wa habari mjini Istanbul kwamba endapo masuala ya usalama hayakushughulikiwa kwa hatua madhubuti ndani ya kipindi maalum, mchakato wa Sweden na Finnland kujiunga na NATO hauwezi kuendelea. Uturuki inasema haikubaliani na uwanachama wa mataifa hayo kwa NATO, ikitaja msimamo wa mataifa hayo kukisaidia chama cha Kikurdi na makundi mengine ambayo Ankara inayachukulia kuwa hatari kwa usalama wake. Miongoni mwa masharti ambayo Uturuki imeyatowa ni kurejeshwa kwa watuhumiwa 28 wa ugaidi kutoka Sweden na wengine 12 kutoka Finnland.