Urusi kuruhusu meli za kigeni kuondoka bandari za Bahari Nyeusi

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imeahidi kufunguwa njia salama za kuzipisha meli za kigeni kuondoka kwenye bandari za Bahari Nyeusi. Mkuu wa Kituo cha Udhibiti wa Ulinzi wa Taifa cha Urusi, Mikhail Mizintsev, amesema njia nyengine itafunguliwa kuruhusu meli kuondoka mji wa bandari wa Mariupol kupitia Bahari ya Azov hadi Bahari Nyeusi. Kwa mujibu wa Mizintsev, kuna meli 70 kutoka mataifa 16 ya kigeni kwenye bandari sita za Bahari Nyeusi, zikiwemo Odesa, Kherson na Mykolaiv. Mapema jana, jeshi la Urusi lilisema bandari ya Mariupol imeanza tena kufanya shughuli zake baada ya miezi mitatu ya mapigano. Jeshi hilo, ambalo lina kituo chake ndani ya Bahari Nyeusi, limefanikiwa kuzuwia meli za kibiashara katika bandari za Ukraine kwa muda wote wa mapigano hadi sasa. Hali hiyo imehatarisha usambazaji chakula duniani, kwani Ukraine ni msafirishaji mkubwa wa ngano, mahindi na mafuta ya alizeti.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii