Homaya nyani husababishwa na virusi vya nyani, kirusi wa familia moja ya virusi vya ndui, ingawa sio kali sana na wataalamu wanasema uwezekano wa kuambukizwa ni mdogo.
Inatokea zaidi katika sehemu za nchi za Afrika ya kati na magharibi, karibu na misitu ya kitropiki.
Kuna aina mbili kuu za virusi - Afrika Magharibi na Afrika ya Kati.
Wagonjwa wawili kati ya walioambukizwa nchini Uingereza walisafiri kutoka Nigeria, kwa hivyo kuna uwezekano kwamba wanaugua aina ya virusi vya Afrika Magharibi, ambayo kwa ujumla ni ndogo, lakini hii bado haijathibitishwa.
Kisa cha tatu kilikuwa mfanyakazi wa afya ambaye alipata virusi kutoka kwa mmoja wa wagonjwa.
Kesi nne za hivi karibuni - tatu huko London na moja kaskazini-mashariki mwa Uingereza - hazina uhusiano wowote unaojulikana, au historia yoyote ya kusafiri. Inaonekana walipata maambukizi Uingereza.
UKHSA inasema mtu yeyote aliye na wasiwasi kwamba anaweza kuambukizwa anapaswa kuona mtaalamu wa afya, lakini awasiliane na wataalamu wa afya kabla ya kufika kituo cha afya.
Dalili za awali ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, uvimbe, maumivu ya mgongo, kuuma kwa misuli na udhaifu wa mwili kwa ujumla.
Mara baada ya homa, upele unaweza kutokea, mara nyingi huanza kwenye uso, kisha kuenea kwa sehemu nyingine za mwili, kwa kawaida viganja vya mikono na nyayo za miguu.
Upele, ambao unaweza kuwasha sana, hubadilika na kupita hatua tofauti kabla hatimaye kutengeneza kipele, ambacho hutumbuka baadaye. Vidonda vinaweza kusababisha makovu.
Maambukizi kawaida huisha yenyewe na hudumu kati ya siku 14 na 21.
Homa ya nyani inaweza kuambukizwa wakati mtu yuko karibu na mtu aliyeambukizwa. Virusi vinaweza kuingia mwilini kupitia ngozi iliyo na jeraha au michubuko, kwa njia ya upumuaji au kupitia macho, pua au mdomo.
Inaweza pia kuenezwa kwa kugusana na wanyama walioambukizwa kama vile nyani, panya na kindi , au kwa vitu kama vile matandiko na nguo.
Hakuna matibabu yake, lakini milipuko inaweza kudhibitiwa kwa kuzuia maambukizi.
Chanjo dhidi ya ndui imethibitishwa kuwa na ufanisi wa 85% katika kuzuia monkeypox, na bado wakati mwingine hutumiwa.