Urusi Yatangaza Kuudhibiti Mji wa Mariupol Wanajeshi Zaidi ya 2,000 wa Ukraine Wajisalimisha

BAADA ya wanajeshi wa Ukraine 531 waliokuwa wamejificha kwenye kiwanda cha Azovstal wakipambana na wanajeshi wa Urusi kujisalimisha, Urusi imemesema kuwa jumla ya wapiganaji 2,439 wa Ukraine sasa wamejisalimisha kutoka eneo hilo katika siku za hivi karibuni.

Moscow haijatoa taarifa zozote kuhusu ni wapi wanajeshi waliojisalimisha Ijumaa wanapelekwa, lakini mabasi ya awali yamepelekwa katika maeneo yanayodhibitiwa na Urusi.

Video iliyotolewa na wizara ya ulinzi ya Urusi, inaonekana ikionyesha msururu wa watu wasio na silaha wakiwakaribia wanajeshi wa Urusi nje ya kiwanda hicho na kujitambulisha kwa rekodi. Kisha kusachiwa na wanajeshi wa Urusi kwa uangalifu.


Maafisa wa Ukraine wanatumai kuwa wanajeshi wake waliojisalimisha na kuwekwa mikononi mwa Warusi wanaweza kuachiliwa kama sehemu ya mpango wa kubadilishana wafungwa lakini hilo halijathibitishwa na Moscow. Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema wanajeshi hao watashughulikiwa “kulingana na sheria husika za kimataifa”, lakini kuna wasiwasi juu ya nini kitatokea kwao ikiwa wataendelea kuzuiliwa na Urusi.

 

Urusi imetangaza ushindi katika mapambano yake ya miezi kadhaa ya kuuteka mji wa bandari wa Mariupol nchini Ukraine. Wapiganaji wa mwisho wa Ukraine waliojibanza katika eneo la kiwanda cha chuma cha Azovstal cha mji huo wamejisalimisha, maafisa wa Moscow wamesema.

 

Kwa miezi kadhaa vikosi hivyo vilikuwa vimezingirwa katika jengo hilo kubwa, na kuizuia Urusi kuwa na udhibiti kamili wa mji huo. Uokoaji wa siku ya Ijumaa unaashiria mwisho wa kuzingirwa na uharibifu zaidi wa mji wa Mariupol ambao sasa umesalia magofu.

 

Mji huo na kiwanda chake cha chuma sasa “umekombolewa kabisa” baada ya wanajeshi 531 wa Ukraine kuondoka katika eneo hilo jana, wizara ya ulinzi ya Urusi imesema.

“Vituo vya chini ya ardhi vya kiwanda hicho, ambako wanamgambo walikuwa wamejificha, viko chini ya udhibiti kamili wa majeshi ya Urusi,” iliongeza katika taarifa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema walinzi wa mwisho waliosalia kaika eneo hilo wameruhusiwa kuondoka.

“Leo wapiganaji hao walipokea ishara ya wazi ya amri ya kijeshi kwamba wanaweza kutoka nje na kuokoa maisha yao,” aliiambia kituo cha televisheni cha Ukraine mapema Ijumaa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii