Biden aanza ziara ya Korea Kusini, Japan

Rais wa Marekani Joe Biden amewasili nchini Korea Kusini leo kwa ziara itakayomfikisha pia nchini Japan inayofanyika chini ya kiwingu cha kutanuka kwa nguvu za China na kurejea kwa majaribio ya silaha nzito nchini Korea Kaskazini. Akiwa mjini Seoul, Rais Biden anatazamiwa kukutana na rais mpya wa Korea Kusini, Yoon Suk-yeol, ambaye tayari ameahidi kuufanya uhusiano kati ya nchi yake na Marekani kuwa imara zaidi hususani kwenye eneo la ulinzi na usalama. Siku ya Jumapili, Biden ataitembelea Japan ambako mbali ya mazungumzo na waziri mkuu Fumio Kishida amepangiwa pia kushiriki mkutano wa kikanda wa kundi la QUAD linazijumuisha Marekani, Australia, India na Japan. Suala la mzozo wa Ukraine, kitisho kutoka Urusi na usalama wa kisiwa cha Taiwan ni miongoni mwa ajenda nyingine muhimu za ziara hiyo ya Biden kwenye mataifa hayo mawili ya mashariki ya mbali ambayo ni washirika wakubwa wa Washington.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii