Mawaziri wa fedha wa nchi wa saba tajiri duniani, wanakutana kwenye mji wa Königswinter, magharibi mwa Ujerumani kujadili mpango wa kuisaidia Ukraine. Mawaziri hao wanajadili namna ya kuuratibisha msaada huo. Waziri wa fedha wa Marekani Janet Yellen amezitaka nchi zote za kundi la G7 ziongeze misaada ya fedha kwa ajili ya Ukraine. Naye waziri wa fedha wa Ujerumani Christian Lindner ametoa wito kwa nchi hizo tajiri kuhakikisha kwamba Ukraine inakuwa na uwezo wa kifedha katika muda wa siku chache zijazo. Wakati huo huo waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida amewaambia waandishi habari kwamba nchi yake itaongeza msaada wa fedha kwa Ukraine hadi kufikia dola milioni 600.