Sweden imepokea hakikisho la kuungwa mkono na Marekani katika kipindi ambapo ombi lake la kutaka kujiunga na Muungano wa Kujihami wa NATO litakapokuwa linazingatiwa na nchi 30 za muungano huo. Haya yamesemwa na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Ann Linde mjini Washington. Sweden na Finland ambazo zimewasilisha maombi hayo, zinahofia usalama wao katika kipindi cha kuidhinishwa kwa maombi yao. Huenda ikachukua hata mwaka mmoja kwa wanachama wa NATO kuidhinisha uanachama wa nchi hizo. Sweden na Finland hazikujiunga na NATO kipindi cha Vita Baridi ila hatua ya Urusi kuvamia na kuinyakua rasi ya Crimea kutoka kwa Ukraine mwaka 2014 pamoja na uvamizi wa sasa wa Ukraine, ni mambo ambayo yamezifanya nchi hizo kutafakari kuhusu sera zao za usalama. Uwezekano wa uanachama wa nchi hizo mbili kukubaliwa katika muungano wa NATO ni mkubwa.