Afisa wa Ukraine na mashirika ya habari ya serikali ya Urusi wamesema kuwa wanawake na watoto kadhaa wamehamishwa kutoka kiwanda cha chuma ambacho ni ngome ya mwisho ya ulinzi ya mji wa bandari wa Mariupol, lakini inaaminika kuwa mamia ya wengine wamesalia maeneo hayo wakiwa na uhaba wa chakula na maji safi. Umoja wa Mataifa ulikuwa ukisuluhisha kuhusu kuhamishwa kwa watu takriban 1,000, wanaoishi katika kiwanda cha Azovstal baada ya majaribio mengi ya hapo awali kushindwa. Ukraine haijasema ni wapiganaji wangapi waliopo kwenye kiwanda hicho, lakini Moscow inakadiria kuwa idadi ya wapiganaji hao ni 2,000. Takriban raia 100,000 bado wamesalia katika mji wa Mariupol.Wakati huohuo Urusi imesema leo katika taarifa ambayo haikuthibishwa na upande wowote huru, kuwa Ukraine inawashambulia kwa mabomu na kuwaua raia wake katika mkoa wa kusini wa Kherson. Serikali ya Ukraine haijajibu tuhuma hizo.