Maelfu ya Wairan wameshiriki kwenye mikutano mikubwa ya maandamano ya umma katika mji mkuu Tehran kuadhimisha siku ya Jerusalem ambayo wanasema ni siku ya kuonesha uungaji mkono wa nchi yao kwa Wapalestina. Ni mara ya kwanza maandamano hayo kufanyika tangu lilipozuka janga la virusi vya corona. Iran imekuwa ikiadhimisha siku hiyo kila ijumaa ya mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhan tangu mapinduzi ya kiislamu mnamo mwaka 1979 yaliongozwa na aliyekuwa kiongozi wa juu nchini humo Imam Ayatollah Ruhollah Khomeini. Siku ya Jerusalem pia inafahamika kama siku ya Quds. Waandamanaji waliokusanyika wamesikika wakizilaani Israel na Marekani. Maandamano hayo yamefanyika pia katika miji mingine ya Iran.