UVIKO-19 Waongezeka Afrika Kusini

Wataalamu wa afya nchini Afrika Kusini wamesema nchi hiyo inashuhudia ongezeko la maambukizo ya ugonjwa wa UVIKO-19 unaosababishwa na aina mpya ya kirusi cha Corona. Mtaalamu wa afya ya umma Salim AbdulKareem ambaye awali alikuwa mshauri wa serikali kuhusu jinsi ya kukabiliana na maambukizo ya UVIKO-19, amesema idadi ya wagonjwa imekuwa ikipungua tangu mnamo Februari ila kutokana na aina mpya ya kirusi cha Corona cha BA.4, maambukizo yameanza kuongezeka tena kwa kasi. Bwana Abdulkareem ambaye ni mtaalamu wa afya ya umma katika chuo kikuu cha Kwa Zulu-Natal amesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wanaolazwa hospitali japo hakuna ongezeko la vifo. Afrika Kusini inarekodi zaidi ya wagonjwa wapya 6,000 wa UVIKO-19 kwa siku, idadi hiyo ikiwa ni ongezeko maradufu tofauti na wiki chache zilizopita. Aina hiyo ya kirusi cha Corona kinaonekana kuwa na nguvu zaidi tofauti na kirusi cha Omicron japo AbdulKareem amesema ni mapema mno kujua iwapo kirusi hicho kipya cha BA.4 kinaweza kusababisha wimbi jipya la maambukizo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii