Ikiwa na miaka sita tangu ianzishwe, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebainisha udhaifu katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato katika Halmashauri ya Ubungo hivyo kushauri hatua za haraka zichukuliwe.
Katika ukaguzi maalumu wa mwenendo wa ukusanyaji wa mapato alioufanya kuanzia 2018/19 hadi 2020/21, CAG amesema halmashauri hiyo ilipata hasara ya Sh4.64 bilioni kutokana na mapungufu iliyokuwa nayo katika ukusanyaji wa mapato.
Tangu ilipoanzishwa, ikimegwa kutoka Manispaa ya Kinondoni mnamo Julai 2016, Kichere amesema Manispaa ya Ubungo ilipewa mgawo wa vyumba saba vya kupangisha vilivyopo Oysterbay Villa katika mitaa ya Mawenzi na Ruvu.
“Licha ya kupewa mgawo huo, Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo haikuwahi kukusanya kodi ya pango katika vyumba hivyo kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2017/18 hivyo kupoteza Sh720 milioni,” amesema Kichere.
Vilevile, Ubungo ilipoteza Sh373.39 milioni katika ushuru wa vibanda na vizimba vilivyopo katika masoko ya halmashauri kutokana na kutoza Sh500 ambayo ni kiwango cha chini cha ushuru kwa siku. Kiwango hicho, hata hivyo, kimeainishwa katika Sheria Ndogo Na. 226 ya Machi 22 mwaka 2019.
Sio hivyo tu, Halmashauri ya Ubungo ilizembea pia katika maeneo mengine yaliyoipotezea mapato muhimu ya kuboresha huduma za wananchi.
CAG anasema halmashauri hiyo imeyaacha maeneo kadhaa wazi bila kuyahudumia na kuweka mazingira rafiki ya kutumika kiasi cha kuvamiwa na wananchi wanaoendesha shughuli zao huku yenyewe ikikosa mapato.
CAG amebaini kuwapo kwa maeneo ya wazi yenye ukubwa wa mita za mraba 69,020 yaliyovamiwa na wananchi ambayo yengeweza kuiingizia halmashauri Sh2.96 bilioni endapo yangekuwa yamepangishwa.
Kiasi hicho kingepatikana iwapo halmashauri ingetoza Sh15,552 kwa mita moja ya mraba kama ilivyoazimiwa kwenye kikao cha kamati ya fedha kilichofanyika Februari 12 mwaka 2019.
Uzembe mwingine ulioinyima halmashauri hiyo mapato, CAG amesema ni kushindwa kusimamia vyema mikataba inayoingia, akitolea mfano ile ya kukusanya ushuru kutoka maeneo tofauti.
CAG amesema halmashauri hiyo ilitoa zabuni mbili za kukusanya ada ya choo katika Kituo cha Mabasi cha Simu 2000 na Soko la Mabibo. Katika zabuni hizo, amebaini halmashauri ilitoa zabuni hizo kwa mawakala walioahidi kiasi kidogo na kuwaacha waliokuwa tayari kuipa fedha nyingi zaidi.
Kichere amesema halmashauri ilimpa mkataba mzabuni aliyesema atatoa Sh131.96 milioni na kumwacha aliyekuwa tayari kutoka Sh207 milioni hivyo kuisababishia upotevu wa Sh75.04 milioni bila sababu za msingi.
Kutoka Kinondoni ilikomegwa, Ubungo imerithi wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao tofauti. Halmashauri hiyo, CAG amesema ilikuwa na wafanyabiashara wakubwa 6,270 wanaostahili kulipa ushuru lakini haikukusanya mapato hayo kwa hao wote.
“Nimebaini halmashauri inadai ushuru wa huduma kutoka kwa wafanyabiashara 38 wakubwa kati ya biashara 6,270 hivyo kujikosesha mapato ya Sh507.52 milioni kinyume na Kifungu cha 6(1) (u) na 7(1) cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 iliyorekebishwa mwaka 2019,” amesema Kichere.
Hasara kwenye mikataba
Katika mwaka wa fedha 2017/18, Halmashauri ya Ubungo ilisaini mkataba wa ujenzi wa jengo la utawala ambao utekelezaji wake ulipaswa kuinufaisha, lakini ikayaacha mapato hayo yaondoke.
Ilipofika Juni 23 mwaka 2020, halmashauri hiyo iliusitisha mkataba huo na mkandarasi aliyekuwapo kutokana na ukiukaji wa masharti uliofanywa na mkandarasi mwenyewe.
Katika mkataba huo uliokuwa na thamani ya Sh6.3 bilioni, CAG amesema halmashauri haikumkata mkandarasi Sh384.31 milioni ambazo ni asilimia 10 ya kazi zilizosalia zilizokuwa na thamani ya Sh2.84 bilioni.
CAG amemshauri katibu mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na katibu tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam kuchukua hatua kuhakikisha fedha hizo zinarudi halmashauri ili ziwanufaishe wananchi wa Ubungo.
“Kwa kushirikiana na mamlaka husika, waliotajwa katika taarifa maalumu wachukuliwe hatua stahiki kwa kuisababishia halmashauri hasara kwa kutofuata sheria na taratibu na vipengele vya mkataba na mawasiliano yafanyike na mkandarasi kuhakikisha Sh284.31 milioni zinarejeshwa,” ameshauri CAG.
Kushindwa kukadiria ushuru
Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa na Sheria ya Fedha ya mwaka 2020, ushuru wa huduma unaolipwa na taasisi au mfanyabiashara binafsi mwenye leseni halali, ni kati ya vyanzo vya uhakika vya mapato vya halmashauri.
Ushuru huu hulipwa na biashara zote ambazo mauzo ghafi yake kwa mwaka yanazidi Sh4 milioni na kila mfanyabiashara au taasisi hutakiwa kulipa kiwango kisichozidi asilimia 0.3 ya mauzo ghafi hayo baada ya kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa bidhaa.
Pamoja na ukweli huo, jambo hilo halisimamiwi kwa ufanisi unaotakiwa na CAG amebaini halmashauri 31, ikiwamo Ubungo hazikukusanya ushuru wa huduma hivyo kupoteza kiasi cha Sh4.57 bilioni kutoka kwa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao ndani ya mamlaka ya halmashauri husika.
Kwa Ubungo, amesema ilishindwa kukusanya zaidi ya Sh141.63 milioni kutokana na kukosekana kwa kanzidata ya wafanyabiashara iliyohuishwa.
“Napendekeza mamlaka za Serikali za Mitaa kuboresha usimamizi wa madeni na kuhakikisha yanajumuishwa katika vitabu vya hesabu za mwisho, kuingizwa katika bajeti na kuacha kulipa madeni ambayo hayamo katika orodha ya wadai iliyoidhinishwa,” ameshauri Kichere.
Mapato kutopelekwa benki
Ingawa fedha zote za Serikali zinapaswa kukusanywa kidijitali kutokana na mifumo iliyofungwa katika halmashauri zote, katika vyanzo ambavyo mifumo hiyo haifiki, mapato yake yanatakiwa kupelekwa benki.
Alipofanya ukaguzi maalumu katika halmashauri tofauti nchini, CAG amebaini Ubungo ilikuwa miongoni mwa halmashauri 31 ambazo zilikusanya Sh9.6 bilioni lakini hazikuzipeleka benki kutokana na udhaifu wa mifumo ya ndani. Fedha hizo, amesema ni makusanyo yaliyofanyika katika mwaka wa fedha 2018/19 hadi 2020/21.
Kati ya kiasi hicho, CAG amesema Sh242.36 milioni zilikuwa makusanyo yaliyofanywa kwenye vituo vya huduma za afya hivyo ameonya kwamba, kutowasilisha mapato hayo benki ni kinyume na Agizo la 50 (5) la Randama ya Fedha za Serikali za Mitaa ya Mwaka 2009 inayoelekeza makusanyo yote kuwasilishwa benki siku hiyohiyo au siku inayofuata.
Kwenye uzembe huu, CAG amesema Ubungo peke yake haikuwasilisha zaidi ya Sh563.07 milioni.
Malipo bila ukaguzi
Kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013 zinaagiza kila taasisi inatakiwa kukagua bidhaa inazonunua na kuzikubali iwapo tu zinakidhi vipimo vilivyowekwa katika mkataba.
Kinyume na hanuni hizo, CAG amebaini mamlaka 21 za Serikali za Mitaa zililipia huduma na bidhaa za Sh2.02 bilioni bila wazabuni kukaguliwa na kamati zilizoteuliwa, ikiwamo Ubungo iliyolipa zaidi ya Sh43.65 milioni kwa wazabuni iliyoihudumia.
“Naishauri Tamisemi kuhakikisha mamlaka zote za Serikali za Mitaa zinafuata sheria husika kwa kuhakiki ubora na kiasi cha bidhaa na huduma kabla hazijapokelewa na kufanya malipo kwa wazabuni,” amependekeza CAG Kichere.
Ukiacha ukaguzi wa huduma au bidhaa, Ubungo imetajwa pia kwenye orodha ya halmashauri ambazo zililipa bila kupima kazi iliyofanyika.
CAG amesema kwenye ukaguzi wake amebaini mamlaka 23 za Serikali za Mitaa zililipa jumla ya Sh3.64 bilioni kwa kazi zilizotekelezwa bila kuwapo nyaraka za vipimo za kazi zilizofanyika. Katika udhaifu huu, amesema Ubungo ililipa zaidi ya Sh81.46 milioni.
Malipo hayo, amesema yalikiuka Kanuni ya 243(2) ya kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013 hivyo kuzitaka taasisi zinazonunua kuidhinisha malipo kulingana na vipimo na uthibitisho kwa kuzingatia hatua zilizoonyeshwa katika mkataba.
Kuidhinisha malipo bila kujiridhisha kiasi kinacholipwa kinafanana na kazi zilizotekelezwa, CAG amesema kunaweza kusababisha malipo ya ziada au malipo ya kazi ambazo hazijatekelezwa hivyo kupoteza fedha za umma.
Ili kukabiliana na udhaifu huo, amependekeza Tamisemi kuhakikisha halmashauri zinapewa wahandisi wenye utaalamu unaohitajika kutathmini kazi zilizotekelezwa na wakurugenzi wa halmashauri hizo kuongeza udhibiti utakaohakikisha kazi zilizokamilika zinathibitishwa kabla ya kulipwa.