TANZANIA na Misri ziko katika hatua ya
mwisho ya majadiliano ya kuipatia ufumbuzi changamoto ya utozaji kodi
mara mbili kwenye bidhaa zinazoingia au kutoka katika nchi hizo mbili
ili kusisimua biashara na kukuza mauzo nje ya nchi yatakayoongeza
upatikanaji wa fedha za kigeni.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, baada ya kukutana na
kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Dkt. Rania
Al-Mashat, kando ya mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la
Fedha la Kimataifa- IMF, Jijini Washington DC, Marekani.
Bw.
Tutuba alisema kuwa majadiliano ya wataalam wa masuala ya kodi kutoka
pande zote mbili yanaendelea na kuahidi kuwa ndani ya kipindi cha miezi
miwili yatakuwa yamekamilika na kuwashauri viongozi wa juu wa nchi
kuhusu hatua zilizofikiwa ili kuondoa changamoto hiyo kwa lengo la
kuboresha biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Misri.
Kuhusu
uwekezaji na ukuzaji biashara, Bw. Tutuba alimhakikishia Waziri huyo wa
Mambo ya Nje wa Misri, Dkt. Rania Al-Mashat, kwamba Serikali imeweka
mazingira mazuri ya uwekezaji na kutoa wito kwa kampuni na mashirika ya
Misri kuja kuwekeza Tanzania.
Bw. Tutuba alisema kuwa zira
iliyofanywa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania nchini Misri, iliwezesha kupatikana kwa wawekezaji 120 ikiwemo
kampuni ya kuzalisha vifaa vya umeme zikiwemo transfoma, ya Elsewedy
Electric East Africa.
Katika hatua nyingine, Tanzania imeahidi
kuiunga mkono Misri kuandaa Mkutano wa 27 wa Mabadiliko ya Tabia nchi
unaotarajiwa kufanyika nchini humo wenye lengo la kutafuta fedha,
teknolojia na uweseshaji kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za
mabadiliko ya tabianchi hususan katika nchi za Afrika.
Kwa upande
wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Dkt. Ranai Al-Mashat alisema
kuwa Misri ni mdau mkubwa wa maendeleo wa Tanzania ambapo hivi sasa
Kampuni ya Misri inajenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa kutumia
maji wa Julius Nyerere na kwamba masuala ya hifadhi ya mazingira ni
muhimu yakatiliwa mkazo kwa pamoja.