Katibu Mkuu wa UN yuko Kyiv kwa mazungumzo na uongozi wa Ukraine

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres yuko mjini Kyiv kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Waziri wa Mambo ya Kigeni Dymtro Kuleba. Guterres amepangiwa pia kulitembelea leo eneo ambalo halijafichuliwa, nje ya mji mkuu. Kama tu ilivyokuwa kwenye ziara yake ya wiki hii mjini Moscow, mojawapo ya mada zinazotarajiwa kujadiliwa ni hali katika mji wa bandari wa kusini mashariki Mariupol, ambako wanajeshi wa Ukraine na raia wamezingirwa na jeshi la Urusi. Guterres alimtembelea Rais wa Urusi Vladmir Putin na Waziri wa Mambo ya Kigeni Sergei Lavrov mjini Moscow na kisha akasafiri kwa treni kutoka Poland hadi Kyiv. Umoja wa Mataifa umesema ofisi yake ya kiutu inaunda timu yenye uzoefu kutoka kote ulimwenguni kuongoza shughuli ngumu ya kuwahamisha raia waliokwama kwenye kiwanda cha chuma mjini Mariupol kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii