Kesi ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya muandaaji yawekwa faraghani

Mahakama ya mwanzo mjini Kigali imeamua kuendesha kesi dhidi ya mwandaaji wa shindano la urembo la Rwanda -Miss Rwanda faraghani ili kuwalinda mashahidi, amesema jaji.

Dieudonné Ishimwe, al maarufu Prince Kid, anashutumiwa ubakaji, kuwa na upendeleo kwa misingi ya ngono , na unyanyasaji dhidi ya wasichana wanaowania taji la urembo.

Bw Ishimwe alitarajiwa kukubali au kukana mashitaka katika kesi ya kutaka dhamana hii leo, lakini mara kesi hiyo ilipoanza mwendesha mashitaka aliomba kesi iendeshwe faraghani.

Mwendesha mashitaka alielezea sababu za kesi hiyo kuendeshwa faraghani kuwa ni za kimaadili na kuwalinda mashahidi.

Bw Ishimwe alipinga, akiomba kuwa kesi iendeshwe wazi“ ili umma ufuatilie na kujua matokeo ya kesi ”.

Jaji aliamua kuiweka kesi faraghani , na waandishi wa habari na umma waliagizwa kutoka mara moja ndani ya chumba cha mahakama.

Kesi hii ni moja ya voisa vinavyozungumziwa zaidi na Wanyarwanda katika mitandao ya kijamii.

Wiki iliyopita, Waziri wa utamaduni aliahirisha shindano la Miss Rwanda, wakati mshindi wa taji hilo wa mwaka 2017 Elsa Iradukunda alipokamatwa kuhusiana na kesi ya Bw Ishimwe.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii