Viongozi wakuu wa Finland wamesema hii leo kuwa wanaunga mkono taifa hilo kuomba uanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO hatua inayofungua njia ya kutanuka kwa muungano huo wa kijeshi baada ya kuongezeka kwa kitisho kutoka Urusi. Katika tangazo la pamoja rais Sauli Niinisto na waziri mkuu Sanna Marin wamesema uamuzi huo unamaanisha Finland iko tayari kuomba kuwa mwanachama wa NATO ingawa italazimika kwanza kukamilisha masharti kadhaa kabla ya kuanza rasmi mchakato huo. Viongozi hao wamesema wanaamini uanachama wa NATO utaimarisha usalama wa Finland na wametoa mwito wa kuharakisha suala hilo baada ya kukamilika kwa mashauriano ya kitaifa ikiwemo ndani ya bunge na vyama vya siasa. Finland ambayo kwa miongo kadhaa imejizuia kuchukua upande katika miungano ya kijeshi imeshuhudia mabadiliko ya maoni ya umma kuhusu sera hiyo tangu Urusi ilipoivamia kijeshi Ukraine.