Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Urusi Sergei Lavrov amekutana na rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune mjini Algiers jana usiku wakati wa ziara yake kwenye taifa hilo la kaskazini mwa Afrika ambalo ni mshirika wa Moscow kwa muda mrefu. Lavrov ameitembelea Algeria katika kilele cha miaka 60 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili huku dhima ya ziara hiyo ikitajwa kuwa ni kuimarisha zaidi mahusiano katika nyanja zote ikiwemo masuala ya kijeshi na yale kibinadamu. Mwanadiplomasia huyo wa Urusi amesema kuwa amemwarifu rais Tebboune juu ya kile kinachoendelea katika vita kati ya Urusi na Ukraine na kusifu msimamo wa Algeria na mataifa ya Kiarabu yaliyojizuia kuchukua upande kwenye vita hiyo. Haijafahamika mara moja iwapo wawili hao walizungumzia suala la nishati ya gesi ikitiliwa maanani kuwa mataifa mengi ya Ulaya yanaizingatia Algeria kuwa chanzo kipya cha nishati kuachana na utegemezi wa Urusi.