Papa Francis aahirisha ziara yake Lebanon

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameahirisha ziara yake nchini Lebanon iliyokuwa imepangwa kufanyika mwezi Juni mwaka huu kutokana na sababu za kiafya. Taarifa hiyo imetolewa jana Jumatatu na waziri wa utalii wa Lebanon Walid Nassar. Nassar hakufafanua sababu hizo lakini papa amekuwa akikabiliwa na maumivu katika goti la mguu wake wa kulia ambayo yamemlazimu kufuta shughuli zake kadhaa na hata kushindwa kusimamia baadhi ya misa na sherehe za kidini. Makao makuu ya Kanisa Katoliki Vatican hayajasema rasmi tatizo linalomkabili papa lakini duru zimeliambia shirika la habari la afp kwamba anaugua ugonjwa wa baridi yabisi. Ziara ya papa nchini Lebanon ingekuwa ya tatu kuwahi kufanywa na kiongozi wa kanisa Katoliki tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya 1975 na 1990.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii