Seneta wa zamani wa Haiti anakabiliwa na mashitaka nchini Marekani kuhusiana na mauaji ya rais wa zamani wa Haiti Jovenel Moise. John Joel Joseph amepandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika mahakama ya shirikisho huko Miami. Raia huyo wa Haiti alipelekwa Marekani kutokea Jamaica Ijumaa iliyopita kujibu mashitaka ya kula njama ya kufanya mauaji au kuteka nyara nje ya Marekani na kutoa msaada wa nyezo uliosababisha kifo, akifahamu au akinuia kwamba nyenzo hizo zingetumiwa kuandaa au kufanya mauaji au kuteka nyara. Seneta huyo wa zamani anakabiliwa na kifungo cha maisha jela iwapo atatiwa hatiani. Joseph na wengine wakiwemo raia 20 wa Colombia na raia kadhaa wa Marekani wenye asili ya Haiti walishiriki njama ya kumteka nyara au kumuua rais wa Haiti ambaye aliuliwa nyumbani kwake Julai 7 mwaka uliopita.