Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy anasema raia 60 wameuwawa wakati shambulizi la bomu la Urusi lilipoiharibu kabisa shule moja katika eneo la mashariki la Luhansk. Maafisa wamesema raia takriban 100 walikuwa katika vyumba vya chini vya jengo hilo katika kijiji cha Bilohorivka wakati liliposhambuliwa. Wakati haya yakiarifiwa viongozi wa nchi tajiri zilizostawi kiviwanda za G7 wanasema wataiwekea vikwazo zaidi Urusi kuhusiana na uvamizi wake nchini Ukraine. Taarifa ya kundi hilo imesema wanataka kufuta au kupiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka Urusi. Viongozi wa G7 wamesema wataimarisha vikwazo dhidi ya matajiri na jamaa wa familia wanaomuunga mkono rais wa Urusi Vladimir Putin katika vita vyake. Marekani imetangaza vikwazo vipya dhidi ya televisheni tatu za Urusi na wakuu wa benki mbili za nchi hiyo.